Breaking News
recent

Zitto: Hali ya uchumi ya watu wetu hapa Tanzania ni mbaya sana

Hali ya Uchumi ya Watu Wetu ni Mbaya Sana

- Mrejesho wa Ziara ya Kiongozi wa Chama Kwenye Kata Zinazoongozwa na ACT Wazalendo

A: Utangulizi

Kati ya tarehe Februari 19 hadi Machi 13, 2018, Kiongozi wa Chama, ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto akiwa pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa, alifanya ziara ya kutembelea Madiwani katika kata mbalimbali nchini, zinazoongozwa nasi ACT Wazalendo kwenye 8, ya Pwani, Morogoro, Arusha, Manyara, Mwanza, Tabora na Kigoma.

Ziara hii ni mwendelezo wa utekelezaji wa kipaumbele Namba 4 cha ACT Wazalendo kwa mwaka 2018 kinachotaka Chama chetu kutetea na kupigania sera za kiuchumi zinazowajali watu wanyonge, tumeamua kuanza na utekelezaji wa kipaumbele hicho katika maeneo tunayoyaongoza.

Malengo mahsusi ya ziara hii ni pamoja na; kuwashukuru wananchi kwa kuipa dhamana ACT kuwaongoza, kushiriki shughuli za maendeleo katika kata, kuzungumza na kamati za maendeleo katika kata, kuzungumza na wananchi husika katika kata, kuangalia utendaji wa madiwani kutokana na matarajio ya wananchi, kuona vikwazo na changamoto za madiwani wetu, kusisitiza uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala yote ya kata, pamoja na kufanya tafiti juu ya masuala ya kisera pamoja na miradi ya maendeleo ambayo ACT Wazalendo Taifa tunaweza kuyabeba kusiadia madiwani wetu.

B: Hali ya Maisha ya Wananchi ni Mbaya Sana

Ziara hii imetuonyesha kuwa hali ya maisha ya wananchi vijijini ni mbaya sana. Kwenye kata zote ambazo tumetembelea tumekuta tatizo kubwa ni hali mbaya ya kipato, migogoro ya Ardhi, kukosekana kwa huduma ya Maji safi na salama, ukosefu wa huduma bora za afya, tatizo la Miundombinu ya Usafirishaji, ukosefu wa pembejeo za Kilimo, ukosefu wa masoko ya mazao ya wavuvi, wakulima na wafugaji, kushuka kwa bei ya mazao yao, kupanda kwa gharama za maisha ya watu, kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi, upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa, vyoo pamoja na walimu, na kuzorota kwa hali ya usalama wa wananchi pamoja na mali zao, hali mbaya ya ajira kwa vijana pamoja na uminywaji mkubwa wa demokrasia na uhuru wa watu kukusanyika na kujieleza.

Hali hiyo inawiana na takwimu zote za kinchi zinazoonyesha kuwa maisha ya WATU wetu yamekuwa mabaya zaidi ndani ya miaka hii miwili ya Serikali ya awamu ya 5, mifano michache ifuatayo inaonyesha hali hiyo:

1. UFUKARA: Kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer wa REPOA, 76% ya Watanzania wana ufukara wa kipato kwa sasa, kulinganisha na 64% ya mwaka 2014. Hivyo basi, ndani ya miaka hii miwili ya utawala huu, mafukara wameongezeka kwa 12%. Hivyo kwa sasa zaidi ya robo 3 ya Watanzania ni mafukara zaidi. Hawa hawana uwezo kabisa wa kulipia huduma za afya, kununua mbegu bora, kunua mbolea, kula mlo bora nk.

2. NJAA: Kwa mujibu wa utafiti huo wa REPOA, 27% ya Watanzania wanalala na njaa sasa kulinganisha na chini ya robo ya Watanzania wanaolala na njaa mwaka 2014.

3. UDUMAVU: Tatizo hilo la njaa linaonekana zaidi kwa kuongeza kwa hali ya udumavu nchini. Mwaka 2011 42% ya watoto wa Tanzania walikuwa wamedumaa, Idadi hiyo ya waliodumaa ilishuka mpaka 34.4% mwaka 2015, kwa sasa imepanda na kufikia 34.7 %. Katika kila watoto 10 nchini walio chini ya miaka mitano, basi watoto wanne (4) wamedumaa kwa sababu ya Lishe duni. Watoto wenye udumavu huu hawanufaiki kabisa na elimu bure inayotolewa.

4. VIFO VYA UZAZI: Kwa mujibu wa ripoti ya Tume ya Takwimu ya Taifa, NBS iliyotoka wiki 2 zilizopita, Vifo vitokanavyo na UZAZI vimepanda kutoka 438/ 100,000 (kwa vizazi salama) hadi 556/100,000. Likiwa ni ongezeko la vifo 118 zaidi. Hali hii inatisha.

5. AJIRA: Utafiti wa REPOA umeonyesha hali ya ajira ni mbaya sana, 31% tu ya Watanzania ndio wanaona Serikali inazalisha ajira kwa sasa, tofauti na 43% walioona hivyo mwaka 2014. Na hili ni kielelezo cha biashara nyingi zilizofungwa tangu utawala wa awamu ya 5 uingie madarakani, kiasi zaidi ya 69% ya Watanzania wanaona Serikali haina uwezo wa kuzalisha ajira na wamekatishwa tamaa. Wengi wa hawa ni vijana, waliomaliza vyuo mbalimbali bila kuajiriwa, tunazalisha bomu litakalotulipukia.

6. MAJI: Kwa mujibu wa Utafiti wa REPOA, Watanzania wanaona upatikanaji wa Maji ni tatizo zaidi sasa kuliko zamani, 42% wanaona maji ni tatizo kubwa ukilinganisha 34% ya mwaka 2014. Ukosefu huu wa maji safi na salama unachagiza maradhi, unapunguza muda wa uzalishaji wa Wananchi, na unavunja ndoa.

7. UFUKARA WA MAJI VIJIJINI: Wastani wa Pato la Taifa la Mtanzania ni shilingi milioni 2.1. Mwananchi wa Kata ya Gehandu, Manyara ananunua maji pipa moja la lita 200 kwa 7000/-, familia yenye watu 6 inahitaji angalau pipa moja kwa siku kwa matumizi ya kujibana kabisa ya maji. Kwa hiyo, familia hii itahitaji takribani shilingi 2.5 milioni kwa mwaka kwa ajili ya Maji tu, hivyo basi, wastani wa 16% ya kipato cha kila mwanafamilia (hata mtoto mdogo wa siku 1) hutumika kununua Maji. Miji mingi nchini kwetu hupata maji kutoka mamlaka za Maji safi na salama. Wastani wa bei ya maji kwa pipa la lita 200 kwa mamlaka za maji nchini ni shilingi 300 tu. Mwananchi wa Uzunguni jijini Arusha au Mikocheni jijini Dar es Salaam au Shanty Town Manispaa ya Moshi au Capri Point jijini Mwanza hutumia wastani wa shilingi 108,000 kwa mwaka kama gharama za Maji kwa familia yake. Familia ya watu 6 ya mjini inatumia chini ya 1% ya wastani wa kipato cha familia kununua maji.

8. VIWANDA NA SEKTA BINAFSI: Ripoti za BoT zinaonyesha Uzalishaji wa bidhaa za Viwandani umeshuka kwa zaidi ya nusu, hata mauzo ya bidhaa za viwandani yameshuka, kutoka trilioni 1.5 mpaka bilioni 700. Mbaya zaidi, tangu mwaka huu uanze viwanda kadhaa vimefunga/kusitisha uzalishaji kutokana na kukosekana kwa sukari ya viwandani pamoja na kutolipwa kwa Ritani zao la Kodi zitokanazo na hiyo Sukari ya Viwandani (pamoja na Ritani za VAT). Viwanda vikubwa viwili vya Saruji vikiwa navyo vimesitisha uzalishaji, na kufanya gharama za bidhaa hiyo kupaa zaidi. Hivyo kuua ndoto nzima ya uchumi wa Viwanda.

9. BEI - NAFAKA: Bei ya mazao ya Wakulima imeshuka mno. Mwaka 2017, Mkulima wa Kata ya Tomondo, Mikese, Morogoro alipata mifuko 10 ya Saruji (cement) kwa kuuza gunia 1 tu la Mahindi (Gunia ilikuwa ni shilingi 120,000 na Mfuko mmoja wa Saruji wa kilo 50 ulikuwa ni shilingi 12,000). Kwa sasa Mkulima huyo anapata mifuko ya Saruji 3.5 akiuza Gunia lake 1 la Mahindi (Gunia sasa ni shilingi 50,000 na Saruji sasa ni shilingi 14,000). Mwaka 2017 Mkulima wa Maharagwe wa Kata ya Msambara, Kasulu, Kigoma aliuza kilo 7.5 za maharagwe na kupata fedha za kununua mfuko mmoja wa Saruji (kilo ya Maharagwe ilikuwa shilingi 2000 na Mfuko wa Saruji ulikuwa shilingi 15,000). Kwa sasa, Mkulima huyo atapaswa kuuza kilo 14.6 za Maharagwe ili kupata mfuko 1 wa Saruji (Maharagwe 1kg ni shilingi 1300 na Saruji ni shilingi 19,000).

10. BEI - MIFUGO: Mwaka 2017 Mfugaji wa Kata ya Sumbugu, Misungwi, Mwanza, aliuza Ng’ombe 1 ili kununua mifuko 27 ya Saruji (Ng’omne mmoja ilikuwa ni shilingi 400,000/- na mfuko mmoja wa Saruji ulikuwa ni shilingi 15,000/-). Kwa sasa, Mfugaji huyo anapata mifuko 9 tu kwa kuuza ng’ombe mmoja (Ng’ombe mmoja ni shilingi 150,000/- na mfuko mmoja wa Saruji ni shilingi 17,000/-).

11. BEI - MAZAO YA BIASHARA: Utafiti wa Mwezi Januari, 2018 uliofanywa na taasisi za Tanzania Pulses Network na East Africa Grain Council unaonyesha kuwa hasara iliyopatikana kutokana na mbaazi zilizokosa soko hapa nchini ni zaidi ya shilingi Bilioni 100. Hasara hii ni kubwa mno kwa wakulima wa mikoa ya Kusini na Pwani. Hasara hii pia iko kwa wakulima wa Giligilani na Pareto katika mkoa wa Manyara ambao bei ya mazao yao imeshuka kwa zaidi ya nusu. Hasara hiyo pia ipo kwa Wakulima wa Tumbaku wa Tabora ambao tumbaku yao imekosa soko kabisa na kudumbukizwa kwenye ufukara.

12. MBOLEA IMEPANDA BEI: Pamoja na matatizo yote hayo ya kupungua kwa tija kwenye Kilimo (kukosekana kwa soko na kushuka kwa bei kwa mazao), Serikali imeamua KUWANYONGA zaidi wakulima, kwa kupandisha bei ya mbolea. Bei elekezi mpya ya Mbolea ya Serikali imepanda kutoka kati ya 41,00/- na 54,000/- mpaka kati ya 47,000/- na 57,000/- kwa mfuko wa 50kg. Jambo hili litawaumiza zaidi wakulima wetu na kuzidisha Ufukara wao. Tangu hapo kuna unyonyaji kwenye sekta ya mbolea, mfano mbolea ambayo bei elekezi ni shilingi 41,000 - 54,000, inauzwa mtaani kwa wastani wa shilingi 60,000 - 85,0000. Sasa badala ya Serikali kuhakikisha inakesha huu unyonyaji, nayo imeamua kuwanyonga zaidi wakulima.

C: Maeneo Makhsus Yanayogusa Maisha ya Wananchi

Migogoro ya Ardhi na Barabara ya Kikeo

Kwenye kata nyingi zilizotembelewa, migogoro ya ardhi kati ya watumiaji wadogo wa ardhi na wawekezaji imechomoza mara kwa mara. Kiini kikuu cha migogoro hii ni ukikwaji wa sheria unaofanywa na watendaji wa serikali wenye dhamana ya kutekeleza sheria ya ardhi na kutokufanyika kwa mpango bora wa matumizi ya Ardhi za vijiji. Hii inasababisha wanaotajwa kama wawekezaji katika vijiji kugawiwa maeneo ya wananchi ya uzalishaji.

Aidha uhifadhi umekuwa ukiingilia ardhi za vijiji na kuchukua maeneo makubwa ya vijiji katika baadhi ya vijiji na kusababisha adha kwa wananchi kunyang’anywa ardhi zao, mazao na mifugo huku wakipigwa kwa kisingizio cha kuvamia maeneo ya hifadhi na baadhi yao kutozwa faini kubwa.

Mifano hai inapatikana katika kata za Mbwawa, Kibaha (Mwekezaji vs Wananchi), Tomondo, jimbo la Morogoro Kusini (Agape Mwekezaji Vs Wananchi), Kata ya Bugaga Kasulu (Kanisa vs Wananchi) Msambara Kasulu (Serikali/Uhifadhi vs Wananchi) na Kata ya Buhigwe jimbo la Buhigwe (Mwekezaji vs Wananchi).

Pia, Katika maeneo mengi tuliyopita kwenye ziara yetu umekuta kero ya miundombinu ya barabara. Wananchi wamelalamikia ukosefu wa barabara zinazopitika kipindi chote cha mwaka. Hii inawasababishia ugumu wakulima kufikisha mazao yao sokoni au kufikiwa kwa urahisi na wafanyabiashara wa mazao.

Kutokana na ubovu wa barabara gharama za usafirishaji zimekuwa kubwa hivyo wafanyabiashara hununua mazao ya wananchi kwa bei ya chini kufidia gharama zao za usafiri. Vilevile imekuwa vigumu kwa wananchi kufuata huduma za muhimu maeneo zinakopatikana hasa miji karibu, huduma hizo kama hospitali, masoko, pembejeo nk. Na hivyo bidhaa zinakuwa vigumu kupatikana kwa urahisi kwao.
Pamoja na ubovu wa barabara tuliouona maeneo mengi lakini kata ya Kikeo, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro tatizo hili ni kubwa kuliko kata nyingine zote, kwani wao hawana barabara kabisa. Katika kata hii tumekutana na changamoto kubwa ya barabara. Wananchi wa kata hii hawajawahi kuwa na barabara tangu dunia iumbwe na wao kuishi kwenye mabonde yale ya safu ya milima ya uluguru.

Wananchi wa Kikeo, kwa msaada mkubwa wa Diwani wao anayetokana na ACT Wazalendo, wanachimba barabara zao kwa mikono na nguvu zao wenyewe. Mwaka jana ndio kwa mara ya kwanza pikipiki zimeweza kufika kwenye vijiji vya Muhale na Chohero baada ya kazi yao ya kuchonga barabara kwa majembe. Wananchi wa Kikeo wanalima Maharage yanayouzwa kwenye soko la kimataifa Nyandira lakini huwabidi kubeba kichwani bidhaa zao kwenda sokoni, jambo ambalo ni mateso makubwa sana. Hali hii kama chama imetugusa.

Uminywaji wa Demokrasia

Ziara yetu kwenye kata tunazoziongoza ilibughudhiwa sana na vyombo vya dola. Jeshi la polisi na baadhi ya watendaji wa serikali walihaha sana kuingilia na kujaribu kuikwamisha ziara yetu. Kilele cha jitihada hizi ni kukamatwa na kulazwa kwangu rumande Mkoani Morogoro usiku wa kuamkia Machi 23, 2018 nikiwa Kata ya Kikeo, Mvomero, Morogoro, kuzuiliwa kutembelea miradi ya maendeleo kwenye kata za Vumilia - Urambo na Usinge - Kaliua mkoani Tabora, pamoja na kuzuiwa kabisa hata kufanya mkutano wa ndani na Diwani wetu katika Kata ya Luale, Mvomero, mkoani Morogoro.

Vitendo hivi vya Jeshi la Polisi kutuzuia kutekeleza wajibu wetu wa kuwaletea wananchi maendeleo kwenye kata tunazoziongoza havikubaliki, ni muendelezo wa kuminya Demokrasia kwa watawala waoga.

D: Hatua Zilizochukuliwa na ACT Wazalendo.

1. UCHUMI: Tumejipanga kupeleka bungeni mpango mbadala juu ya Sera za Kibajeti za nchi yetu kwa sasa, kwa kupinga mpango wa sasa wa bajeti unaojikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya watu. Masuala tutakayoyasimamia ni Uchumi Shirikishi unaozalisha Ajira, kwa kuhakikisha Kilimo pamoja na Viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya Kilimo ndio kipaumbele kikuu, Usalama wa Chakula na Lishe, pamoja na huduma bora za Kijamii, hasa Maji, Elimu na Afya.

2. ARDHI: Tumemwandikia barua, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ndugu Lukuvi aingilie suala hili. Licha ya juhudi tunazoziona za Waziri kushughulikia migogoro ya ardhi, sisi ACT Wazalendo tunaamini kuwa Serikali kwa kiasi kikubwa inashirikiana na watu wenye fedha kupora ardhi za wananchi wanyonge. Tumeitaka Serikali itazame upya namna ya kushughulika na migogoro ya ardhi, na tumetaka wananchi kupewamashamba pori yote ambayo wawekezaji waliyapora kutoka kwa wananchi.

3. MAJI: ACT Wazalendo tumeamua kutumia mfumo wa PPP, kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa kushirikisha Sekta Binafsi na Serikali za Vijiji katika Kata tunaziongoza, kwa kuwa na miradi ya mfano itakayotatua changamoto hii. Kamati yetu ya Maendeleo ya Jamii tayari imeteua timu ndogo ya kusimamia jambo hili. Timu hiyo, inayohusisha wataalam wa sekta ya maji itatembelea katika kata za Tomondo - Morogoro, Gehandu - Hanang, Sumbugu - Misungwi, Usinge - Kaliua, na Kalinzi - Kigoma Kusini. Lengo letu ni kuwezesha njia mbadala za kutatua kero za wananchi katika maeneo ambayo chama chetu kinadhamana ya kuongoza.

4. USHIRIKA: Tumewahamasisha wananchi katika Kata zote tunazoziongoza ili kujikusanya kwa pamoja na kuunda ushirika wenye nguvu ili kulinda maslahi ya wakulima, wavuvi na na wafugaji, pia kujiunga na mtandao wa vikundi vya wakulima kama MVIWATA ili kupaza sauti zao zaidi. ACT Wazalendo tutahakikisha vikundi husika vya ushirika vinapata mafunzo sahihi ya kujiendesha kwa uwazi, weledi na uadilifu, na pia Kuvihamasisha kujiunga na hifadhi ya jamii ili kuwa na akiba na kupata urahisi wa mikopo ya kujiendeleza.

5. DEMOKRASIA: Tumefungua Kesi ya Madai Na. 8/2018 Mahakama Kuu hapa Dar Es Salaam, kulishtaki Jeshi la Polisi, kutokana na Jeshi hilo kuingilia, visivyo halali shughuli, ziara yetu ya kuhamasisha maendeleo katika Kata tunazoziongoza. Tunaamini Mahakama itatenda haki kwenye suala hili.

6. BARABARA: Tumeamua kama chama kusaidiana na Diwani wa Kata ya Kikeo, kupata jawabu la kero ya barabara ndani ya muda uliobakia kabla ya mwaka 2020. Tayari tumeshamuunganisha Diwani na wafadhili ambao watasaidiana na wananchi kufikisha barabara ya kuunganisha vijiji vya Kata hii na masoko ya bidhaa zao.

7. AFYA NA ELIMU: ACT Wazalendo tutashiriki Ujenzi wa Zahanati, Vituo vya Afya, Madarasa na Nyumba za Walimu. Ingawa wajibu huu ni wa Serikali kwa kuwa ndiyo inayokusanya Kodi, sisi ACT Wazalendo, kupitia falsafa yetu ya ‘Siasa ni Maendeleo’, tunao wajibu wa kuhamasisha mapambano dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini. Hivyo basi hatua hii ya kushiriki ujenzi huu wa miundombinu ya Afya na Elimu ni ili kukabiliana na hali duni tuliyoikuta katika Kata tunazoziongoza. Chama chetu kimefanya tathmini ya mahitaji, na sasa kimejipanga kuhamasisha wanachama, wananchi na wadau wa maendeleo kuchangia mifuko 1,371 ya Saruji (Cement), nguvukazi pamoja na Mabati 2,680 ili vitumike kwenye ukarabati, pamoja na ujenzi wa Vyumba vya madarasa, Nyumba za Walimu, Zahanati na Vituo vya Afya katika kata zote tunazoziongoza.

F. Mapendekezo kwa Serikali

1. Matabaka: Ufanyike Uchambuzi huru wa namna rasilimali za kibajeti za nchi yetu zinavyogawanywa kati ya mijini na vijijini. Hii ni kutokana na ukweli kuwa maisha ya wananchi vijijini ni mabaya mno, hasa kukosekana kwa huduma za msingi kama vile Maji, Barabara, Elimu na huduma za Afya ilhali kuna miradi mikubwa ya mabilioni ya fedha kwenye miji mikubwa nchini. Mfumo huu unaunda matabaka ya Ufukara na Unyonyaji kwenye ugawaji wa Keki ya Taifa. Ni rai yetu kuwa, ni wakati muafaka sasa kwa Taasisi za Utafiti kama REPOA na ESRF zifanye uchambuzi huu na matokeo yake kuwekwa kwa umma ili kupata namna nzuri ya mgawanyo wenye tija wa mapato kati ya vijiji na mijini.

2. Uchumi: Juzi Serikali imeainisha vipaumbele vya Kibajeti kwa mwaka 2018/19, masuala ya watu, kama Kilimo na Maji hayamo kabisa kwenye vipaumbele hivyo, ni rai yetu kwa Serikali ijitazame katika eneo hilo, ikae chini na kuja na mpango mpya unaojikita katika masuala ya watu, na sio huu wa sasa unaojikita kwenye vitu tu. ACT Wazalendo tutahakikisha tunaupinga bungeni mpango huu wa Bajeti ya sasa unaowaacha kando 76% ya Watanzania wote.

3. Demokrasia na Ustawi wa Taifa: Tunaendelea kusisitiza rai yetu kuhusu umuhimu wa kuitisha Mkutano wa Kitaifa wa Maridhiano ya Kisiasa kama jukwaa la kuzijadili changamoto za uendeshaji wa siasa nchini. Jambo hilo litaondoa uadui unaoendelea kukua sasa kati ya Serikali na wananchi, viongozi wa dini, mashiriki yasiyo ya Kiserikali, taasisi za wanafunzi, pamoja na vyama vya Upinzani. Tunaamini mazungumzo ya Kitaifa ndio jambo sahihi la utatuzi wa suala hili.

4. Usalama wa Nchi: Tunapendekeza kuundwa kwa Tume Huru kuchunguza matukio ya Mauaji, Utekwaji na Kupotea kwa Wafanyabiashara, Viongozi wa Kisiasa, Waandishi wa Habari pamoja na wananchi wengine.
5. Uwajibikaji Halmashauri: Wizara ya Tamisemi ihakikishe kuwa katika Halmashauri zinazoongozwa na CCM, maelekezo yake ya kuwa Kamati ya Fedha na Uongozi ya Halmashauri yenye angalau Diwani mmoja kutoka Vyama vya Upinzani yanatekelezwa. Ziara yetu imeonyesha Halmashauri nyingi zinazoongozwa na chama hicho hazifuati agizo hili, na hivyo kuondoa kabisa nafasi ya uwajibishaji na usimamizi kwenye mapato ya Halmashauri.

No comments:

Featured post

ADVANCED ENGENEERING MATHEMATICS

Powered by Blogger.